Ni afueni kwa mbunge wa Mbeere Kaskazini Leo Wamuthende baada ya Mahakama Kuu ya Embu kupuuzilia mbali kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake.
Wamuthende alichaguliwa kuwa mbunge wa eneo hilo baada ya kupata kura 15,802 na kumbwaga mpinzani wake mkuu Newton Kariuki almaarufu Newton Karish wa chama cha DP aliyejizolea kura 15,308 kwenye uchaguzi mdogo ulioandaliwa Novemba 27, 2025.
Kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake iliwasilishwa na Karisha akidai vurugu, utishiaji wa wapiga kura na udanganyifu katika vituo vya kupigia kura uliathiri matokeo ya uchaguzi huo.
Kwenye uamuzi wake, Jaji Richard Mwongo alisema mlalamikaji alikosa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Wamuthende hakuchaguliwa kihalali.
Aidha, mahakama ilisema ushahidi wa kutosha haukuwasilishwa kuthibitisha jinsi vurugu zilivyoathiri matokeo.
Uamuzi huo una maana kwamba Wamuthende ataendelea kuhudumu kama mbunge wa eneo hilo hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 wakati kivumbi kikali kinatazamiwa kushuhudiwa kati ya chama tawala cha UDA na kile cha Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.