Serikali itawaajiri walimu 20,000 mwaka huu, asema Rais Ruto

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto ahudhuria maadhimisho ya miaka 70 ya shule ya upili ya Thika.

Rais William Ruto amesema serikali inalenga kuwaajiri walimu 20,000 mwaka huu 2026, ili kuziba pengo la idadi ya walimu kwa wanafunzi.

Akizungumza leo Ijumaa katika shule ya upili ya Thika, kaunti ya Kiambu, kiongozi wa nchi alisema tangu serikali yake ilipochukua hatamu za uongozi mwaka 2022, imekabiliana na changamoto za ukosefu wa walimu shuleni, kwa kuwaajiri walimu 100,000.

Alisifu mfumo wa elimu wa CBE, akisema unazingatia kikamilifu talanta za kila mwanafunzi huku ukitoa fursa sawa kupitia masomo ya Sayansi, teknolojia, uhandisi na Hisabati (STEM), sanaa na masomo mengine.

Aidha, Rais Ruto alisema takriban asilimia 60 ya wanafunzi kwa sasa wanachukua mkondo wa STEM.

Kulingana na Rais Ruto mfumo wa awali uliotegemea sana mitihani, uliwafanya wanafunzi wengi kuonekana kama waliofeli kwa sababu haukutambua talanta na uwezo wao tofauti.

Rais alisema kuwa mageuzi katika sekta ya elimu hayajahusisha tu mabadiliko ya mtaala, bali pia yameshughulikia changamoto za muda mrefu kama vile wanafunzi wengi madarasani, upungufu wa walimu na ucheleweshaji wa fedha za elimu.

Aliyasema hayo alipoungana na wanafuzi wa zamani, wafanyakazi na wanafunzi wa shule ya upili ya Thika wakati wa maadhimisho ya miaka 70 ya shule hiyo.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetangula, katibu wa Elimu ya Msingi Julius Bitok, Kiongozi wa walio wengi kwenye Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah, Mwakilishi Mwanamke wa Kiambu Muratha, mbunge wa Thika mjini Alice Ng’ang’a na waziri wa zamani Moses Kuria.

Share This Article