DPP amtaka afisa kwenda likizo ya lazima kwa tuhuma za kula hongo

Martin Mwanje
2 Min Read
Japheth Ouko Mayore Isaboke - Kiongozi Mkuu wa Mashtaka eneo la Kilgoris

Japheth Ouko Mayore Isaboke, Kiongozi Mwandamizi wa Mashtaka anayesimamia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ya Kilgoris ameagizwa kwenda likizo ya lazima mara moja kutokana na tuhuma zinazomwandama za kupokea rushwa.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga katika taarifa hiyo amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa mwongozo wa mwaka 2022 wa sera na taratibu za masuala ya wafanyakazi wa ODPP.

Hii ni hadi uchunguzi ambao tayari umeanzishwa juu ya madai dhidi yake utakapokamilishwa.

“ODPP inasisitiza sera yake ya kutokomeza visa vyote vya ufisadi miongoni mwa wafanyakazi wake kwa mujibu wa wito wake wa Mashtaka yenye Haki na Usawa,” ilisema ofisi hiyo.

“ODPP inaahidi kushirikiana na taasisi husika ya upelelezi na inaahidi kuwa hatua mwafaka zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kufungua mashtaka.”

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) leo Jumatatu imetangaza kumkamata Isaboke kwa tuhuma za kuitisha hongo.

Isaboke anadaiwa kuitisha hongo ya shilingi 50,000 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja ili kesi dhidi ya mfanyabiashara huyo iharakishwe.

Baada ya mazungumzo kati yao, fedha hizo zilipunguzwa hadi 40,000.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alikataa kulipa rushwa hiyo na badala yake kuripoti suala hilo kwa EACC.

EACC  ilifanya operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa mashtaka jana Jumapili wakati akipokea sehemu ya hongo hiyo yenye kima cha shilingi 20,000.

Mshukiwa alizuiliwa katika kituo cha polisi cha  Kisii na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 30,000 pesa taslimu akisubiri uchunguzi kukamilika.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *