Washukiwa watatu wanaohusishwa na wizi wa Spring Valley wakamatwa

Watatu hao walikamatwa baada ya polisi kutekeleza operesheni  katika eneo la Githurai Mwiki, kaunti ya Kiambu, ambapo bastola mbili zikiwa na risasi zilipatikana.

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa watatu wanaohushiwa na wizi wa Spring Valley wakamatwa.

Maafisa wa Polisi wamewakamata washukiwa watatu wanaodaiwa kuhusika na visa vya uhalifu katika kaunti ya Nairobi na viunga vyake.

Watatu hao walikamatwa baada ya maafisa hao kutekeleza operesheni  katika eneo la Githurai Mwiki, kaunti ya Kiambu, ambapo bastola mbili zikiwa na risasi zilipatikana.

Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, washukiwa hao wamehusishwa na wizi wa kimabavu ulionaswa kwenye kamera za CCTV katika eneo la burudani katika barabara ya General Mathenge, eneo la Spring Valley kabla ya kutoroka kutumia pikipiki.

Maafisa wa uchunguzi wa maeneo ya uhalifu (CSI), walikusanya ushahidi ambao utafanyiwa uchunguzi wa kisayansi, huku washukiwa hao wakizuiliwa wakisubiri kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.

Mshukiwa mwingine anayedaiwa kuhusika kwenye wizi huo aliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi katika mtaa wa Joska, juma lililopita.

Huduma ya Taifa ya polisi imerejelea kujitolea kwake kusambaratisha mitandao yote ya wahalifu , kuhakikisha wale wote wanaohusika na uhalifu wanachukuliwa hatua za kisheria.

Share This Article