Watatu wakamatwa na EACC Igembe Kaskazini kwa ubadhirifu wa fedha

Waliomakatwa ni Pauline Waruguru Mwangi, James Muroki Eusebio na James Ntonjira Ntongai huku mshukiwa mwingine, Joshua M'maroo, akitakiwa kujisalimisha.

Martin Mwanje
2 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewakamata washukiwa watatu kuhusiana na madai ya ubadhirifu wa shilingi milioni 4.8 katika eneo bunge la Igembe Kaskazini. 

Fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ununuaji na uwekaji wa transfoma 6 za umeme chini ya Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) ya eneo bunge hilo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Waliomakatwa ni Pauline Waruguru Mwangi, James Muroki Eusebio na James Ntonjira Ntongai.

Watatu hao wamepangiwa kuwasilishwa katika mahakama ya Meru ili kusomewa mashtaka.

EACC inasema ilianzisha uchunguzi kufuatia madai ya ubadhirifu wa shilingi milioni 4.8 uliofanywa na maafisa waandamizi wa NG-CDF ya eneo bunge la Igembe Kaskazini wakati wa kipindi cha fedha cha mwaka 2014/2015.

“Uchunguzi ulibaini kuwa kamati ya NG-CDF ya Igembe Kaskazini ilipokea shilingi milioni 4.8 kwa ajili ya ununuaji na uwekaji wa transfoma sita katika maeneo ya Buathine, Ethiopia, Ntobocui, Luciuti MCK, Marere Centre, na Murune, huku kila transforma ikitengewa shilingi 800,000,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud kwenye taarifa.

“Tume ilibaini kuwa fedha hizo zilihamishiwa kwenye akaunti sita za mradi na kutolewa siku hiyo na waweka sahihi ambao ni James Muroki Eusebio, James Ntonjira Ntongai na joshua M’maroo, kwa agizo la Meneja wa Hazina ya NG-CDF wakati huo, Pauline Waruguru Mwangi.”

Uchunguzi ukibaini kuwa ingawa kamati hiyo ilidai kuhusisha Mamlaka ya Usambazaji Umeme Mashambani (REA) na kampuni ya umeme, KPLC kutekeleza mradi huo, taasisi hizo mbili zilithibitisha kuwa hazikupokea malipo yoyote wala mawasiliano kuhusu manunuzi.

“Hakuna transfoma zilinunuliwa wala kuwekwa popote katika maeneo yaliyotambuliwa ya mradi huo,” iliongeza EACC.

Punde baada ya kukamilika kwa uchunguzi, tume iliwasilisha faili ya uchunguzi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ambaye aliidhinisha kushtakiwa kwa Mwangi, Eusebio, Ntongai na M’maroo kwa mashtaka mbalimbali, ikiwa ni pamoja na njama ya kujihusisha katika ufisadi na utumizi mbaya wa mamlaka.

EACC imetoa wito kwa M’maroo kujisalimisha kwa ofisi ya tume hiyo ya kanda ya mashariki.

 

 

 

Share This Article