Asilimia 57 ya wakazi wa Ol Kalou walijitokeza kupiga kura

Martin Mwanje
1 Min Read

Asilimia 57 ya wapiga kura 73,480 katika eneo bunge la Ol Kalou walijitokeza kumchagua mbunge wao mpya wakati wa uchaguzi mdogo ulioandaliwa jana Alhamisi. 

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwenye taarifa imewashukuru wakazi hao kwa kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki ya kidemokrasia.

Ni nadra idadi kama hiyo ya wapiga kura kujitokeza wakati wa uchaguzi mdogo nchini.

“Tume inakariri kwamba uchaguzi wa kuaminika unahitaji ushirikiano na nia njema kutoka kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na vyama vya kisiasa, asasi za usalama, watawala, mashirika ya kijamii, vyombo vya habari na umma,” imesema IEBC kwenye taarifa.

“Uaminifu katika uchaguzi wetu unajengwa siyo tu kupitia ubora wa kiufundi lakini pia uwajibikaji wa pamoja wa wadau wote ili kulinda uadilifu wa mchakato huo.”

IEBC sasa inasema itarejelea mchakato wa kusajili wapiga kura wapya katika eneo bunge la Ol Kalou punde baada ya kukamilika kwa muda wa kukata rufaa ya kupinga matokeo hayo.

Kwenye uchaguzi huo, Sammy Ngotho wa chama cha DCP aliibuka mshindi baada ya kuzoa kura 35,440 huku mpinzani wake mkuu Samuel Muchina Nyagah wa UDA akifuata kwa mbali baada ya kupata kura 5,450 pekee.

Uchaguzi huo ulivutia jumla ya wagombea 9.

Share This Article