Red Cross yapokea vifaa vya matibabu kutoka WHO

Afisa Msimamizi wa WHO Kenya Chipo Takawirana, alikabidhi vifaa hivyo kwa Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya Dkt. Ahmed Idris.

Tom Mathinji
1 Min Read
Red Cross yapokea vifaa vya matibabu kutoka WHO

Shirika la Msalaba Mwekundu Nchini Kenya, limepokea vifaa vya matibabu kutoka Shirika la Afya Duniani, vitakavyotumika katika utoaji huduma za matibabu kwa watu zaidi ya 60,000 ambao wameachwa bila makao katika kaunti ya Marsabit.

Msaada huu unalenga kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya matibabu kufuatia wimbi la wakimbizi waliovuka mpaka kuingia Moyale tangu mwezi Oktoba kutokana na ukosefu wa usalama.

Afisa Msimamizi wa WHO Kenya Chipo Takawirana, alikabidhi vifaa hivyo kwa Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya Dkt. Ahmed Idris.

“Vifaa hivi vya matibabu vitawezesha maafisa wetu na wale wa Wizara ya Afya kuwahudumia jamii, huku mahitaji ya matibabu yakiongezeka,” alisema Idris.

Msaada huo unajumuisha vifurushi 46 vya dharura vya afya, vikijumuisha vifurushi 30 vya dharura vifurushi 10 vya vifaa tiba, na vifurushi 6 vya dawa za ziada pamoja na vifaa vya kukabiliana na malaria.

Kulingana na shirika la Red Cross, dawa na vifaa hivi vinatosha kuhudumia takriban watu 30,000 kwa muda wa miezi mitatu, pamoja na vifaa vya ziada kwa ajili ya watu 10,000 katika kambi za ulinzi na jamii zinazowahifadhi.

Share This Article