Bunduki 12 haramu zimesalimishwa kwa hiari kwa maafisa wa polisi katika Kaunti Ndogo ya Samburu Magharibi.
Silaha hizo zilikabidhiwa kwa maafisa wa polisi katika Kituo cha Polisi cha Loosuk siku ya Ijumaa, hii ikiwa ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kutwa silaha inayomilikiwa kinyume cha sheria ili kurejesha amani na usalama katika eneo hilo.
Kupitia kwa taarifa, Huduma ya Taifa ya Polisi imesema bunduki zote 12 zimehifadhiwa salama, zikisubiri hatua zaidi za kiutawala.
Wakati huo huo ikiwapongeza wananchi waliojitokeza kusalimisha silaha hizo na kuwahimiza wakazi wengine wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kufuata mkondo huo, ili kufanikisha utangamano kwa njia ya amani.
Wananchi wamehimizwa kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kuripoti shughuli zozote za kutiliwa shaka katika kituo cha polisi kilicho karibu.