Lissu apendekezwa kuwania tuzo ya Sakharov

Lissu ambaye ni mwanasheria na mwanasiasa nchini Tanzania, amewekwa kwenye orodha ya wagombea wa Tuzo hiyo akiwa mahabusu kwa tuhuma za uhaini.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu .A. Lissu, amependekezwa kuwa mmoja wa wawaniaji wa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, inayotolewa na Bunge la Ulaya.

Tuzo hiyo kubwa ya Bunge la Ulaya hukabidhiwa watu, makundi au mashirika yanayotambuliwa kwa mchango wao katika kutetea haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na demokrasia.

Lissu ambaye ni mwanasheria na mwanasiasa nchini Tanzania, amewekwa kwenye orodha ya wagombea wa Tuzo hiyo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, akiwa mahabusu kwa tuhuma za uhaini.

Pendekezo la jina la Lissu limetolewa na kundi la kisiasa la European People’s Party, EPP katika mchakato wa mwaka huu, hatua inayoiweka Tanzania katika mjadala mpana wa kimataifa kuhusu haki za kisiasa, utawala wa sheria na nafasi ya upinzani katika demokrasia.

Kwa mujibu wa taarifa ya EPP, uteuzi huo unahusishwa na historia ya Lissu katika kutetea mageuzi ya kidemokrasia na haki za msingi
nchini Tanzania, pamoja na changamoto binafsi alizokabiliana nazo katika shughuli zake za kisiasa na kijamii.

Tuzo hiyo, inayojulikana kama Sakharov Prize for Freedom of Thought, imekuwa moja ya alama muhimu za Bunge la Ulaya katika kutambua watu na taasisi zinazopigania uhuru wa mawazo na haki za binadamu duniani.

Viongozi wa Afrika waliowahi kutunukiwa tuzo hiyo ni pamoja na Nelson Mandela Rais wa zamani wa Afrika Kusini, aliyetuzwa mwaka 1988 tuzo hiyo ilipoanzishwa akishinda pamoja na Anatoly Marchenko akiwa bado gerezani, kwa mapambano yake dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Hauwa Ibrahim, Mwanasheria wa haki za binadamu wa Nigeria, alishinda tuzo hiyo mwaka 2005 baada ya kutetea wanawake na vijana waliokuwa wakikabili hukumu kali chini ya sheria za dini ya kiisilamu almaarufu Sharia.

Denis Mukwege ambaye ni Daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya wanawake wa asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alishinda tuzo hiyo mwaka 2014, kwa kuwahudumia waathiriwa wa ubakaji wa halaiki na ukatili wa kingono uliotumiwa kama silaha ya vita.

Share This Article