Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amefungua rasmi Kongamano na Maonyesho ya nne ya Mwaka ya Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi katika Chuo Kikuu cha Strathmore jijini Nairobi.
Mudavadi ametilia mkazo ulinzi wa wafanyakazi wahamiaji na kuimarisha upatikanaji wa haki za kazi.
Kongamano hilo la siku tatu, lina kaulimbiu ‘Uhamiaji wa Wafanyakazi na Upatikanaji wa Haki: Kuimarisha Mwitikio wa Mahakama kwa Mifumo Jumuishi na Yenye Ufanisi ya Haki za Kazi’.
Mudavadi alisema fursa kwa Wakenya wanaotafuta ajira nje ya nchi zinapaswa kufungua njia za kuboresha maisha bila kuwaweka katika hatari ya kunyanyaswa.
Alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha uhamiaji wa wafanyakazi unakuwa salama, halali na unaungwa mkono na mifumo inayolinda haki na heshima ya wafanyakazi.
Mkuu huyo wa mawaziri aliwahimiza Wakenya wanaotafuta ajira nje ya nchi kuthibitisha fursa hizo kupitia njia rasmi za serikali, ikiwemo Wizara ya Kazi, Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira na Idara ya Nchi ya Masuala ya Diaspora.
Alisema serikali itaendelea kuimarisha ulinzi wa kisheria na kitaasisi ili kuwawezesha Wakenya kutafuta ajira nje ya nchi kwa ujasiri zaidi.
Jaji Mkuu wa ELRC Monica Mbaru aliwakaribisha Mudavadi, Waziri wa Kazi na Ulinzi wa Jamii Alfred Mutua na Katibu wa Masuala ya Diaspora Roselyn Njogu katika kongamano hilo.
Mijadala katika kongamano hilo inahusu mwenendo wa uhamiaji wa wafanyakazi, uhamaji wa wafanyakazi, migogoro ya ajira inayovuka mipaka, viwango vya kimataifa vya kazi, haki za binadamu na utawala wa kikatiba.
Washiriki pia watajadili mikakati ya mahakama kuhusu haki ya wakimbizi kufanya kazi nchini Kenya na katika mataifa mengine.
Kongamano hilo linawaleta pamoja wadau wakuu katika sekta ya haki za kazi kwa lengo la kuimarisha uwezo wa mahakama na mifumo ya kitaasisi katika kushughulikia mahitaji ya wafanyakazi wahamiaji.