Wahalifu 1,189 wa ghasia za kisiasa wamehukumiwa tangu 2022

Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen alisema adhabu zilizotolewa na mahakama zilitofautiana kulingana na uzito wa makosa.

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, amefichua kwamba watu 1,189 wamehukumiwa kwa makosa yanayohusiana na ghasia za kisiasa na uhalifu wa makundi ya vijana tangu mwaka 2022.

Murkomen alisema adhabu zilizotolewa na mahakama zilitofautiana kulingana na uzito wa makosa.

Alisema serikali imejitolea kukabiliana na vitendo vya kihuni na ghasia za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Hii ni sehemu ya ushahidi kwa wale wanaosema polisi hawafanyi lolote kuwakamata wahuni,” alisema.

Murkomen alikuwa akizungumza mbele ya bunge la Seneti alipokuwa akijibu maswali ya maseneta kuhusu masuala mbalimbali ya usalama wa taifa na utoaji wa huduma za serikali.

Waziri huyo pia alithibitisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Hatari za Maafa wa 2025–2030, pamoja na hatua nyingine za kukabiliana na majanga na dharura za kitaifa, ikiwemo mvua ya El Niño inayotarajiwa.

“Kituo cha Kitaifa cha Operesheni za Maafa kinaendelea kuratibu maandalizi na mwitikio wa maafa katika ngazi ya kitaifa kwa kutumia mfumo unaohusisha serikali nzima na jamii nzima,” alisema Waziri.

Murkomen pia alisisitiza kuwa nchi iko salama, akisema serikali imepiga hatua kubwa katika kukabiliana na vitisho vya usalama na inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za serikali kote nchini.

Share This Article