Viongozi wa nchi mbali mbali za Afrika wameanza kuwasili jijini Nairobi kwa ajili ya kongamano la ustawi wa Afrika linaloandaliwa katika jumba la KICC kesho na Jumanne.
Aliyetanguliwa kuwasili nchini ni Rais wa Côte d’Ivoire Alassane Ouattara, aliyewasili usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.
Rais Ouattara alilakiwa na Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano kabla ya mkutano huo mkuu wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Ufaransa na mataifa ya Afrika, unaoandaliwa katika taifa lisilozungumza kifaransa kwa mara ya kwanza.
Rais Julius Maada Bio wa taifa la Sierra Leone, naye aliwasili mapema leo na kulakiwa vile vile na waziri Miano huku Rais wa Liberia Joseph Nyuma Boakai naye akiwasili muda mfupi uliopita na kupokelewa na Maurice Okoth.
Kongamano hilo litawakutanisha wakuu wa Nchi za Afrika, Viongozi wa sekta ya biashara, Vijana na wanaharakati ambapo wataangazia kuimarishwa kwa ushirikiano wa Ufaransa na Afrika.
Wahudhuriaji wa kongamano hilo wataangazia pia njia za kuendeleza mazungumzo kuhusu biashara na uwekezaji kati ya sehemu nyingi za maslahi sawa.
Ufaransa ilinzisha makongamano ya ushirikiano na mataifa ya Afrika rasmi mwaka 1973 wakati Rais Georges Pompidou alikuwa madarakani, na tangu wakati huo, makongamano yamekuwa yakiandaliwa nchini Ufaransa au katika mataifa yanayotumia lugha ya kifaransa barani Afrika.
Rais wa sasa wa Ufaransa Emmanuel Macron, amekuwa akitafuta kujenga tena ushawishi wake barani Afrika ndiposa mikutano kama hii inaandaliwa.