Kenya imeshirikiana na mataifa jirani kuimarisha uchunguzi na ufuatiliaji wa maradhi katika maeneo ya mipakani na kubadilishana taarifa katika juhudi mpya za kuzuia kuenea kwa michipuko hatari ya magonjwa katika kanda hii.
Akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa Nairobi na uliowaleta wadau wa afya kutoka nchi 11 kujadili mkakati utakaoimarisha utayari wa dharura za afya, Katibu wa afya ya umma Mary Muthoni, alisema hatua hiyo inalenga kuboresha utayari wa kukabiliana na changamoto ibuka za afya, kupitia ushirikiano wa karibu wa kikanda.
“Tunachunguza huduma muhimu za afya ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya hata nyakati za dharura hususan kwa jamii za mpakani,” alisema Muthoni.
Kulingana na Muthoni, mataifa hayo yanakamilisha mfumo wa kikanda utakaowezesha kushirikisha taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa kwa wakati halisi, kuratibu uchunguzi wa afya mipakani na kuimarisha mwitikio wa pamoja wakati wa dharura.
“Dharura za afya hazitambui mipaka. jukumu letu la pamoja ni kubuni mifumo dhabiti itakayofanikisha kuzuia, kutambua na kushughulikia dharura za afya, huku tukiendelea na utoaji wa huduma muhimu,” alidokeza katibu huyo.