Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, ametoa wito kwa wakazi wa eneo la Mlima kenya kumuunga mkono Naibu Rais Kithure Kindiki, akisema anawakilisha mustakabali wa uongozi wa eneo hilo.
“Nawasihi mumuunge mkono Prof. Kindiki kama Naibu Rais,” alisema Murkomen.
Akizungumza katika kaunti ya Embu wakati wa hafla ya kutoa shukrani katika shule ya upili ya St. Stephen, Murkomen alipuuzilia mbali madai ya hivi majuzi kwamba Kindiki anakabiliwa na changamoto ndani ya serikali, akidokeza kuwa changamoto kuu inaweza kuwa iwapo atakosa ungwaji mkono kutoka eneo hilo.
“Hakuna tatizo na Prof. Kindiki. Atakuwa na tatizo ikiwa hamtamuunga mkono,” alidokeza waziri huyo.
Wakati huo huo, Murkomen aliwahakikishia wananchi usalama na udhabiti, akisema serikali inajizatiti kukabiliana na wahuni.
“Napongeza Huduma ya Taifa ya polisi. Katika mikutano ambayo imetekelezwa katika muda wa wiki mbili zilizopita, hakujakuwa na visa vya uhuni,” alisema Murkomen.
Alisema serikali haitavumilia shughuli zozote za uhalifu zinazolenga kuhatarisha usalama kote nchini.
“Hatutamkubalia yeyote kubeba silaha akidai anajilinda huku akizua ghasia,” alionya Murkomen.
Murkomen aliongeza kuwa wizara yake imetekeleza mageuzi ya polisi yanayokusudiwa kuwapa wafanyakazi wa usalama ujuzi wa kisasa ili kuwawezesha kupambana na vitisho vinavyoibuka vya usalama katika anga ya kidijitali.
Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Katibu wa Vyuo vya kiufundi na Mfunzo Dkt. Esther Muoria, Alex Wachira (Nishati), Betsy Njagi (Uchumi Samawati na uvuvi), na Mhandisi Joseph Mbugua (Barabara).
Wengine ni Seneta wa Embu Alexander Mundigi, Wabunge Muchangi Karemba (Runyenjes), Mhandisi Nebart Muriuki (Mbeere Kusini), na wawakilishi wadi miongoni mwa wengine.