Hospitali ya Msambweni yapigwa jeki

Dismas Otuke
2 Min Read

Idadi ya watoto wachanga wanaopata matibabu maalum katika hospitali ya rufaa ya Msambweni Kaunti ya Kwale imeongezeka hadi 90 kwa mwezi kufuatia upanuzi na ufunguzi wa kituo cha watoto wachanga wanaohitaji matibabu maalum katika hospitali hio.

Kituo hicho kilichojengwa kupitia ushirikiano wa Serikali ya Kaunti ya Kwale na Wakfu wa M-Pesa, kimepunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto za kiafya.

Gavana wa Kaunti hiyo Fatuma Achani anahoji kuwa serikali ya kaunti hiyo imepiga hatua katika uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi zikiwemo kupatikana kwa huduma za dharura katika hospitali ya Msambweni, zikiwemo chumba cha wagonjwa mahututi,mtambo wa oksigeni,kituo cha kuhifadhi damu pamoja na huduma za upigaji picha kwa kina mama wajawazito (CT Scan) ili kukinga kina mama na watoto kupoteza maisha.

Aidha Achani ameongezea kuwa Serikali ya Kaunti ya Kwale imeweza kujenga na kufungua vituo 178 vya afya katika Kaunti hiyo vinavyotoa huduma za afya ya uzazi.

Naye Edith Mwasi ambaye ni Daktari Mkuu wa Maswala ya watoto hospitalini humo na Betty Wambughu Nesi mkuu wa maswala ya afya ya uzazi wamesema tangu ufunguzi wa vituo hivyo wanaweza kulaza wagonjwa wengi kwa wakati mmoja na pia kupunguza msongamano katika vyumba vya awali hatua ambayo imechangia kupungua kwa vifo vya kina mama na watoto.

Serikali ya Kaunti ya Kwale imepiga hatua katika uboreshaji wa sekta ya afya ikiwemo kupandisha hadhi hospitali ya Mkongani, Kinango,Samburu,Kwale na LungaLunga hadi daraja la nne kuhakikisha wakaazi hawataabiki kutafuta huduma za afya.

Share This Article