Wanafunzi 9 wa shule ya wasichana ya Utumishi kuzuiliwa kwa siku 21

Upande wa mashitaka uliifahamisha mahakama kuwa michakato muhimu ya kisayansi ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa DNA, bado haijakamilika.

Tom Mathinji
2 Min Read
wanafunzi 9 wa shule ya wasichana ua utumishi kuziliwa kwa siku 21.

Wanafunzi tisa wa shule ya wasichana ya  Utumishi wanaoshukiwa kuteketeza bweni na kusababisha vifo vya wanafunzi 16, watazuiliwa kwa siku 21, kutoa fursa kwa maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi.

Huku ikikubali ombi la kiongozi wa mashtaka, mahakama ya Naivasha ilisema uchunguzi kuhusu mashtaka ya mauaji na uteketezaji unaendelea na unahitaji muda zaidi ili kuukamilisha.

Upande wa mashitaka uliifahamisha mahakama kuwa michakato muhimu ya kisayansi ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa DNA, bado haijakamilika.

Zaidi ya hayo, upande wa mashitaka ulidokeza kuwa, kuzuiliwa kwa wanafunzi hao sio tu muhimu kwa uadilifu wa uchunguzi, lakini pia ni muhimu kwa ulinzi wao, kutokana na hisia za umma zinazozingira kesi hiyo.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Naivasha  Abdulqadir Ramadhan, aliagiza kuwa wanafunzi hao wazuiliwe katika makao ya watoto ya Nakuru katika kipindi hicho cha siku 21.

“Wakati wa kipindi cha kuzuiliwa watapata fursa ya kutembelewa na maafisa kutoka idara ya watoto kuhakikisha haki zao zinalindwa,” alisema Ramadhan.

Hakimu Mkuu huyo aidha, aliwazuia wanahabari na umma kuwapiga picha au kuchapisha habari zozote kuhusu wanafunzi hao.

Wakati huo huo, mahakama iliagiza kuwa wanafunzi hao wapewe fursa ya kupata  huduma za wakili na huduma nyinginezo muhimu wakati wa kipindi cha kusikilizwa kwa kesi dhidi yao.

Kesi hiyo itatajwa Juni 24, 2026 kwa maelekezo zaidi pamoja na kupokea hatua za uchunguzi zilizopigwa.

Share This Article