Wanafunzi watundu kukiona cha mtema kuni, aapa Waziri Ogamba

Waziri amesema serikali inachukulia kwa uzito suala la vurugu na utovu wa nidhamu kwa jumla shuleni.

Martin Mwanje
2 Min Read

Wanafunzi wote watakaopatikana wakizua vurugu na kujihusisha katika vitendo vya utovu wa nidhamu shuleni wataadhibiwa vikali kwa mujibu wa sheria. 

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Elimu Julius Ogamba wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatanao.

“Serikali inachukulia kwa uzito suala la vurugu na utovu wa nidhamu kwa jumla shuleni. Haijalishi una malalamishi kiasi gani, kamwe hakuwezi kuwa na sababu ya kusababisha kifo na kuharibu mali,” aliashiria Waziri Ogamba.

“Malalamishi yote yanapaswa kuangaziwa kupitia njia zifaazo bila kugeukia vitendo visivyokubaliwa kisheria wala vurugu. Wahusika wote watakabiliwa vikali kwa mujibu wa sheria.”

Ogamba alirejelea kisa cha mkasa wa moto uliotokea katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru mwishoni mwa mwezi uliopita, akikitaja kuwa cha kusikitisha mno.

Alidokeza kuwa uchunguzi umebaini kuwa mkasa huo ulikuwa kitendo cha uchomaji moto kimakusudi kilichoanzishwa na baadhi ya wanafunzi.

“Washukiwa 9 tayari wamefikishwa mahakamani na wanazuiliwa. Tunatuma risala za rambirambi kwa familia za wale waliowapoteza wapendwa wao na kuwatakia majeruhi nafuu ya haraka,” aliongeza Waziri Ogamba.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo kumekuwa na wimbi la vurugu na visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi katika baadhi ya shule za sekondari nchini kiasi cha kusababisha shule hizo kufungwa kwa muda usiojulikana.

 

Share This Article