Jumla ya shule 204 zilifungwa kutokana na vurugu za wanafunzi ambazo zimeshuhudiwa katika siku za hivi karibuni kote nchini.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba amesema nyingi ya shule zilizoathirika ni zile za sekondari ya juu.
“Hadi sasa, tumepokea ripoti za vurugu zinazoathiri shule za sekondari ya juu 204 kote nchini. Tayari, wanafunzi wa shule 59 kati ya shule hizi wamerejea shuleni na kuendelea na masomo yao, huku wengine zaidi wakiendelea kurejea,” amesema Ogamba.
“Wanafunzi katika Gredi za 1 hadi 9 wanaendelea na masomo yao, bila matatizo makubwa yaliyoripotiwa. Kwa hivyo, mfumo wetu wa msingi wa elimu unaendelea vizuri, isipokuwa matatizo yaliyoshuhudiwa katika shule za malazi za sekondari ya juu kama nilivyotaja.”
Kulingana na Waziri Ogamba, tathmini yao inaashiria ni asilimia 2 pekee ya shule za sekondari ya juu zilizoathiriwa na vurugu kote nchini ikiashiriwa kuwa masomo yanaendelea vyema katika asilimia 98 ya shule hizo.
Kwa mantiki hiyo, amewapongeza wanafunzi wengi kwa kutojihusisha katika visa vya vurugu alivyosema serikali imedhamiria kuviangamiza kabisa nchini.
Ameahidi kuwa serikali itabuni jopo linalowatela pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya elimu kubaini chanzo cha misukosuko iliyoshuhudiwa shuleni na njia bora za kukabiliana nayo.
Aidha, muda wa likizo utasalia Juni 24-28 kama ilivyopangwa.
Wazazi wametakiwa kutumia muda huo kutangamana na watoto wao na kuwapa ushauri ipasavyo ili kusaidia kuepusha visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwao.
Kwa upande mwingine, shule zimetakiwa kuimarisha hatua za usalama na kusuluhisha malalamishi yoyote yanayowasilishwa na wanafunzi haraka iwezekanavyo.