Shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) na lile la Qatar Airways, zimetia saini mkataba wa makubaliano, kwa lengo la kuongeza safari za ndege kati ya Nairobi na Doha.
Mkataba huo uliotiwa saini na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Airways Allan Kilavuka na mwenzake wa Qatar Mhandisi Badr Mohammed Al-Meer, utawezesha shirika la ndege la Qatar, kuanzisha safari ya tatu ya kila siku ya ndege kati ya Doha na Nairobi.
Aidha kupitia makubaliano hayo, mashirika hayo mawili yatashirikiana katika uunganishaji wa safari za ndege na kuwapa fursa wateja wao kuwa na uwezo mkubwa wa kuchagua safari zao kote duniani.
Akizungumza wakati wa kutia saini mkataba huo, Kilavuka alisema ushirikiano huo unawiana na mkakati wa mageuzi katika shirika la KQ ambao umelisababisha kupata faida katika muda wa zaidi ya mwongo mmoja mapema mwaka huu.
“Ushirikiano huo utafanikisha juhudi za KQ za kuimarisha utalii na uchukuzi wa mizigo na kupiga jeki ukuaji wa uchumi kwa Kenya na kanda ya Afrika Mashariki kwa Jumla,” alidokeza Kilavuka.
Kwa upande wake, Mhandisi Mohammed Al-Meer, alisema Kenya inarekodi nzuri ya ushirikiano Barani Afrika, akidokeza kuwa shirika la ndege la Qatar litaendelea kuchangia katika ukuaji wa uchukuzi wa ndege na uchumi wa mazingira.
“Ushirikiano huu ni dhihirisho la uhusiano ulioimarika katika kanda ya Afrika,”alisema afisa huyo.