Rais William Ruto amehamisha taasisi ya ubunifu ya Kenya kutoka wizara ya elimu hadi ofisi ya Rais.Rais alisema hatua hii itasaidia katika kubuni nafasi za kazi.Akiongea wakati wa maadhimisho ya wiki ya ubunifu ya Kenya ya mwaka 2024 katika kituo cha mikutano cha Edge,Rais alisema bajeti ya kutosha na vile vile mwongozo wa sera zinahitajika katika kusaidia kuanzisha kampuni kubwa zinazoweza kutoa ajira kwa vijana zaidi.Alisema serikali inatumia mikakati kutoa nafasi za ajira kwa vijana.
Rais alisema Kenya inatoa mchango mkubwa kwa mpango wa marekebisho ya kiuchumi barani Afrika sambamba na ajenda ya mwaka 2063 na vile vile katika kiwango cha dunia.Rais Ruto alisema uwekezaji wa Kenya katika kawi safi ni dhihirisho tosha la kujitolea kwa nchi hii kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.
Serikali imeunganisha kebo za fiber optic za umbali wa kilomita elfu-13 kote nchini katika utekelezaji unaoendelea wa mradi wa kuimarisha uchumi wa kidijitali wa taifa hili. Katibu katika idara ya teknolojia ya habari,mawasiliano nas uchumi dijitali mhandisi . John Tanui alisema muundombinu huo wa ziada utatekelezwa ili kuafikia lengo la umbali wa kilomita laki-1 mraba katika awamu ya kwanza iliyotekelezwa mwaka 2023 na inatarajiwa kukamilishwa kufikia mwaka-2028. Tanui aliongeza kwamba kufikia sasa uunganishaji umeimarishwa,hali inayopunguza haja ya kusafiri ili kupata habari na huduma,kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa gezi na kufanikisha utoaji huduma kwa wananchi.
Katika mwezi Aprili mwaka-2023, bodi ya wakurugenzi wa Shirika la benki duniani waliidhinisha ufadhili wa awamu ya kwanza wa dolla bilioni -390 za Marekani kufanikisha mradi huo. Mradi huo unanuiwa kutanua upatikanaji wa huduma za intaneti ya hali ya juu,kuimarisha ubora wa elimu na huduma muhuimu zilizochaguliwa za serikali pamoja na kukuza ujuzi kwa ajili ya uchumi wa kidijitali katika kanda hii ambapo imewezesha kebo za umbali wa kilomita elfu 13 kuunganishwa. Benki ya dunia iliidhinisha dolla milioni-180 zaidi za marekani zitakazotumika katika utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.
Waziri wa Leba Alfred Mutua alikabiliwa na kibarua kigumu pale ambapo vijana waliohudhuria awamu ya kwanza ya mchakato wa ajira wa kitaifa katika Kaunti ya Baringo, walitaka kujua ni kwa nini serikali inalenga kuwasafirisha wakenya nje ya nchi badala ya kuboresha uchumi wa taifa. Waziri huyo alikuwa akifuatilia mchakato wa utoaji ajira wa kitaifa katika juhudi za kuwapeleka wafanyakazi katika mataifa ya Dubai, Saudi Arabia na mataifa mengine ya mashariki ya kati. Hata hivyo vijana hao walitoa wito kwa serikali ya kitaifa na kaunti kujenga viwanda na kuweka mazingira bora ya ustawi wa biashara badala ya ajira katika mataifa ya nje.
Katika utetezi wake, Dkt. Mutua alisema taifa kwa sasa lina idadi kubwa ya wafanyakazi kuliko kiwango inachoweza kuajiri, huku njia pekee ya kushughulikia changamoto hiyo ikiwa ni kutafuta nafasi za ajira nje ya nchi. Akizungumza katika ukumbi wa chuo cha kitaifa cha mafunzo anwai cha Baringo wakati wa zoezi la uajiri, waziri huyo aliwahakikishia vijana hao kujitolea kwa serikali, kuhakikisha haki na uwazi wakati wa mchakato huo, na kuonya kuwa shirika lolote linalojihusisha na vitendo vya udanganyifu litakabiliwa kisheria.
Wataalamu wa ununuzi wa bidhaa na huduma wanategemea ongezeko la matumizi ya teknolojia katika kupambana na ufisadi katika usambazaji wa bidhaa ambao kwa kiasi kikubwa umelaumiwa kwao. Wataalamu hao wana matumaini kwamba matumizi ya teknolojia katika ununuzi wa bidhaa na huduma za umma na za kibinafsi, kutaongeza uwazi na kurahisisha ufuatiliaji na ukaguzi wa michakato ya zabuni. Akizungumza wakati wa kongamano la 3 kuhusu ugavi wa bidhaa kitaifa katika hoteli ya Sarova Whitesands katika Kaunti ya Mombasa, mwenyekiti wa taasisi ya usimamizi wa ugavi nchini KISM John Karani, aliridhia matumizi ya teknolojia kuboresha usimamizi wa ugavi nchini.
Hazina ya kitaifa ilianza kufanya majaribio ya mfumo wa ununuzi wa serikali ‘EGP’ kuanzia Jumatatu wiki hii. Mkurugenzi wa ununuzi wa hazina ya kitaifa Eric Korir, alisema mfumo wa EGP unaofanyiwa majaribio, utaimarisha vita dhidi ya ufisadi kwani utafanya michakato ya ununuzi kuwa wazi zaidi.
WIZARA YA AFYA YAZINDUA WARSHA YA UHAMASISHAJI
Wizara ya afya imezindua warsha ya siku tatu ya uhamasisho dawa na mbinu za kukabiliana na matumizi ya Mihadarati ikiwemo tumbako. Warsha hiyo inayoandaliwa katika chuo cha sayansi na teknolojia cha Meru, kilicho kaunti ya Meru inanuiwa kuhamasisha umma kuhusu athari za matumizi mabaya ya dawa na mihadarati.Akiongea wakati wa uzinduzi huo,mwenyekiti wa bodi ya kuthibiti Tumbako Dr. Naomi Shaban alisema matumizi ya tumbako yameongezeka hasa miongoni mwa vijana na kuathiri familia nyingi.
Katika Habari za Kimataifa ni Kwamba: Shughuli ya upigaji kura inaendelea nchini Namibia katika kile kinachotarajiwa kuwa uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi, tangu taifa hilo kujinyakulia uhuru kutoka kwa Afrika Kusini miaka 34 iliyopita. Netumbo Nandi-Ndaitwah analenga kuwa rais wa kwanza wa kike wa nchi hiyo.Anawania urais kwa tiketi ya chama tawala cha South West Africa’s People’s Organisation ‘Swapo’, kuchukua nafasi ya Hage Geingob, ambaye alifariki mwezi Februari baada ya kuwa madarakani kwa miaka tisa. Ukosefu wa ajira, umaskini, usawa na madai ya ufisadi yameathiri uungwaji mkono wa chama hicho. Mpinzani mkuu wa Nandi-Ndaitwah ni Panduleni Itula wa chama cha Independent Patriots for Change ‘IPC’, pamoja na wawaniaji wengine 14. Vyombo vya habari nchini humo vimeonyesha foleni ndefu katika shule na vituo vingine vya kupigia kura wakati upigaji kura ukianza mapema leo asubuhi.
Kwingineko, Shirikisho la Riadha la Boston BAA limesema litalipa pesa za zawadi kwa wanariadha waliomaliza nyuma ya wanariadha waliopatikana na hatia ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwenye mbio zao. Waandalizi wa mbio za marathoni za Boston walisema inapanga kuwasiliana na wanariadha wanaostahili kupata zawadi baada ya matokeo yao kuboreshwa baada ya matokeo ya wanariadha waliomaliza mbele zao kufutiliwa mbali. Mpango huo utaanza mwaka 1986, wakati BAA ilipoanzisha pesa za zawadi. Mbio za marathoni zimekumbwa na visa vingi vya vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika miaka ya hivi maajuzi. Mkenya Diana Kipyokei alivuliwa taji yake ya mbio za marathoni za Boston aliyonyakua mwaka 2021 baadaya kupatikana na hatia ya utumizi wa dawa za kusisimua misuli miaka miwili iliyopita na akapigwa marufuku ya miaka sita. BAA ilisema malipo hayo ya hiari yataanza mwezi Januari na kwamba wanariadha wanaoamini kuwa waliathiriwa wanapaswa kutuma maombi ya kulipwa fidia.