Hukumu ya Lissu: Polisi waonya dhidi ya vurugu

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jummane Muliro amesema wamepokea taarifa za watu kuhamasishana kusafiri hadi Dar siku hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read
Tundu Lissu, Kiongozi CHADEMA

Maafisa wa polisi nchini Tanzania hususan wale wa Kanda Maalum ya Dar es salaam wameonya dhidi ya vurugu siku ambayo mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu atakuwa anasomewa hukumu.

Polisi hao wameonya vikali, makundi ya watu wanaodaiwa kuhamasishana kufanya vurugu, fujo na vitendo vya uhalifu Ijumaa Novemba 6, 2026, Lissu anapotarajiwa kufahamu hatima yake kwenye kesi ya uhaini.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jummane Muliro amesema wamepokea taarifa kwamba kuna watu ndani na nje ya Dar es salaam wanaohamasishana kusafiri kwenda Jijini Dar siku hiyo, huku baadhi yao wakidaiwa kuwa na nia ya kufanya fujo na vurugu.

Polisi wameelezea kwamba wanatambua haki ya wananchi kufika Mahakamani, wakisisitiza kuwa maeneo ya Mahakama yanajulikana na yana uwezo wa kuhudumia Watu wanaohitaji kufika kwa ajili ya shughuli za kisheria.

Hata hivyo, Polisi wameonya kuwa hawatavumilia Makundi au Watu watakaobainika kupanga au kuhamasisha vurugu, hujuma na vitendo vingine vya kihalifu kwa kutumia siku hiyo kama fursa.

Kesi hiyo ya Lissu imekuwa ikiendelea tangu Aprili 10, 2025, siku moja baada yake kutiwa mbaroni alipokuwa akifanya kampeni ya kuhimiza mabadiliko kabla ya uchaguzi mkuu.

Kakake ambaye alikuwa wakili Allute Mughwai aliaga dunia ghafla usiku wa kuamkia Novemba Mosi, 2026, na familia ikaamua kuahirisha mazishi yake hadi baada ya Tundu Lissu kusomewa hukumu.

Share This Article