Timu ya taifa ya Kenya ya soka ya wanawake Harambee Starlets imeititiga Ushelisheli mabao 11 katika marudio ya raundi ya kwanza kufuzu kwa michezo ya Olimpiki ,mechi iliyochezwa Jumatatu alasiri katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.
Starlets ambao walikuwa wenyeji wa mkondo huo baada ya Ushelisheli kuwaalika Kenya wiki jana katika uwanja wa Ulinzi,walikuwa kifua mbelel mabao 5-0 kufikia mapumzikoni.
Jentrix Shikangwa alipachika mabao mawili nao Sylvia Makungu na Violet Nanjala walifunga bao moja kila mmoja.
Mwanahalima Jereko na Marion Serenge waliongeza mawili kila mmoja katika kipindi cha pili nao Fasila Adhiambo na Shikangwa wakaongeza moja kila mmoja.
Kenya imefuzu kwa raundi ya pili kwa ushindi wa jumla wa magoli 22-0, baada ya kushinda duru ya kwanza 11-0 na watakabiliana na aidha Zimbabwe au Malawi katika raundi ijayo.