Rais William Ruto amezindua ujenzi wa jengo la kuwahudumia wagonjwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Meteitei, kaunti ya Nandi utakaogharimu shilingi milioni 270.
Kulingana na kiongozi wa taifa, hospitali hiyo inalenga kupanua utoaji wa huduma bora za afya kwa maelfu ya wakazi wa eneo hilo.
Jengo hilo la vitanda 50, litaongeza idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutoka 66 hadi 116, huku wagonjwa 350,000, wakitarajiwa kupokea matibabu kutoka katika kituo hicho.
Akizungumza kwenye ziara yake kaunti ya Nandi, Rais Ruto alisema uwekezaji kwenye hospitali na mioundombinu ya umma, ni sehemu ya kujitolea kwa utawala wake kuimarisha utoaji wa huduma na kuhakikisha maendeleo yanatekelezwa katika sehemu zote za nchi.
“Kwa sasa tunaangazia maendeleo. Nimekuja hapa kushughulikia barabara, hospitali, masoko na uunganishaji wa stima,” alisema Rais Ruto.
Upanuzi wa hospital ni mpango mpana wa serikali katika kaunti ya Nandi, kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma muhimu na kuboresha maslahi ya wakazi wa kaunti hiyo.