Serikali imetekeleza ahadi muhimu ambazo ilitoa kwa jamii ya Waislamu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Rais William Ruto ametaja kumaliza ubaguzi wakati wa utoaji wa vitambulisho vya taifa na kuimarisha miradi ya maendeleo.
Alidokeza kuwa ili kutimiza ahadi hizo, alitia saini agizo la kusitisha mchakato uliokandamiza jamii ya Waislamu katika maeneo ya mipakani ya nchi.
“Tuliweka bayana kwamba Wakenya wote wakiwemo Waislamu na jamii zinazoishi katika sehemu za mipakani wana haki ya kupata huduma sawa katika utoaji wa vitambulisho vya taifa na pasipoti na hivyo ndivyo tumefanya,” alisema Rais Ruto.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi Jumatano aliposhiriki mkutano na viongozi wa Waislamu, Ruto aliwahakikishia kuwa kucheleweshwa kutekelezwa kwa hazina ya Waqf, itakuwa tayari kufikia mwezi Septemba mwaka 2026.
Wakati huo huo, Ruto alidokeza kuwa ujenzi wa barabara ya kilomita 750 ya Isiolo-Mandera unaendelea, huku ikilenga kuunganisha jamii zilizotengwa za Kaskazini mwa Kenya na masoko ya kiuchumi na huduma muhimu.