Kituo cha kitaifa cha ambulensi chazinduliwa

Rais Ruto amesema kituo hicho kitatekeleza jukumu muhimu katika kuboresha utoaji wa matibabu ya dharura kwa wanaoyahitaji nchini kote.

Martin Mwanje
1 Min Read

Kenya imepiga hatua katika utoaji wa huduma za dharura kufuatia kuzinduliwa kwa kituo cha kitaifa cha kuratibu huduma za ambulensi cha SHA 922 Lifeline kinacholenga kuokoa maisha wakati wa dharura nchini kote.

Kituo hicho kitakachoendeshwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA kitatumiwa kuwaunganisha wagonjwa na hospitali mbalimbali katika kaunti zote 47 nchini.

Tayari ambulensi na watoa huduma za dharura 1,243 wamepewa kandarasi na SHA ili kutoa huduma chini ya mpango huo.

“Kituo cha Kitaifa cha Ambulensi hakiwapokonyi wamiliki ambulensi hizi. Inafanya rahisi kuzipata, inasaidia kuratibu upelekwaji wake, na kinagharimia kila safari inayostahiki,” alisema Rais wakati wa uzinduzi huo.

“Uzinduzi wa leo huenda usitatue kila mapungufu ya mfumo wetu wa afya ya dharura, lakini unaweka msingi wa huduma ya kitaifa iliyoratibiwa na kutuwekea jukumu la kuuboresha kila wakati.”

Ambulensi zaidi ya 600 zimepelekwa katika kaunti mbalimbali ili kuhakikisha kila Mkenya anayehitaji matibabu ya dharura anapata huduma hizo haraka iwezekanavyo.

Rais Ruto alitumia fursa hiyo kudokeza kuwa Wakenya milioni 32.2 wamejisajili na SHA. Jumla ya Wakenya milioni 8 wamepokea matibabu chini ya SHA huku hospitali, vituo vya afya na zahanati zikilipwa shilingi bilioni 178.5.

 

 

 

 

Share This Article