Naibu Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini Kenya, FKF McDonald Mariga na wanachama sita wanaoegemea mrengo wake, wametimuliwa wakati wa mkutano mkuu maalum wa FKF ulioandaliwa kaunti ya Meru siku ya Jumamosi.
Mariga na wanachama wengine sita wa Baraza Kuu,NEC walitimuliwa kwa kukiuka sheria na katiba ya FKF.
Mkutano huo mkuu maalum ulicheleweshwa kwa muda baada ya maafisa wa polisi kurusha vitoza machozi ndani ya ukumbi.
Saba hao walioenguliwa ni pamoja na Mariga ambaye ni Naibu Rais, Mwanachama wa NEC wa pwani Gabriel Mghendi, Mwanachama wa NEC Nairobi mashariki Daniel Shikanda, Mwakilishi wanawake Violet Kerubo na Mwanachama wa NEC kutoka eneo la kati Robert Kenneth Macharia.
Wengine waliofurushwa ni mwanachama wa NEC kutoka Upper Rift Valley Bernard Korir Lagat na Mwanachama wa NEC kutoka Nyanza Collins Opiyo Kalee.
FKF imesema itatangaza maafisa wapya watakaojaza nafasi hizo siku zijazo.
Maafisa wengi wa polisi walikuwa katika ukumbi wa mkutano kushika doria.