Takriban wauguzi 800 wa Hospitali ya Chuo kikuu Cha Kenyatta ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti (KUTRRH), wamefutilia mbali mgomo wao baada ya kukubaliana na usimamizi wa hospitali hiyo kuhusu maslahi yao na kuimarishwa kwa mazingira ya kazi.
Katibu Mkuu wa chama cha wauguzi na wakunga (KNUNM) Seth Panyako, alitangaza kuwa chama hicho kimeondoa rasmi na bila masharti ilani ya mgomo ya siku 21 baada ya kutia saini Mkataba wa Makubaliano na usimamizi wa hospitali hiyo.
Akizungumza katika hospitali hiyo siku ya Ijumaa, Panyako alisema makubaliano hayo yameshughulikia masuala yote yaliyokuwa kwenye ilani ya mgomo na kutoa fursa kwa kuimarishwa kwa maslahi ya wafanyakazi na utoaji huduma za matibabu bila kutatizwa.
Mkataba huo unaowakilisha wanachama zaidi ya 800, ulitiwa saini na Panyako kwa niaba ya chama hicho huku Afisa Mkuu wa KUTRRH Dkt. Zeinab Gura, akitia Saini kwa niaba ya hospitali hiyo.
Chini ya mkataba huo, marupurupu ya uuguzi, sare na hatari ya kiafya, yameongezwa.