Viongozi wa Magharibi walaani visa vinavyoongezeka vya uhuni

radiotaifa
1 Min Read
Kenneth Lusaka - Gavana wa Bungoma

Baadhi ya viongozi kutoka eneo la Magharibi mwa nchi wanaoegemea mrengo unaotawala wa Kenya Kwanza wamelaani vikali visa vinavyoongezeka vya uhuni nchini.

Wakiongozwa na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, viongozi hao wamewalaumu baadhi ya wanasiasa wanaosema wanawafadhili vijana kusababisha vurugu kwenye mikutano ya kisiasa na kuisha kuilimbikizia serikali lawama.

Wakizungumza katika hafla ya uwezeshaji iliyoandaliwa katika eneo la Kolongolo, kaunti ya Trans Nzoia, wamesema ushindani unapaswa kujikita kwa mawazo, sera na rekodi za maendeleo wala si vitisho na vurugu.

Gavana Lusaka alionya kuwa viongozi wanaochochea vurugu wanatishia demokrasia na kudhoofisha imani ya umma katika mchakato wa kisiasa.

Onyo sawia lilitolewa na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula aliyesema vurugu zinazoshuhudiwa katika ulingo wa kisiasa nchini ni tishio kwa uthabiti wa taifa.

Visa vya uhuni vimeongezeka nchini katika siku za hivi karibuni, cha hivi karibuni kikishuhudiwa katika eneo la Keumbu, kaunti ya Kisii mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo mtu mmoja alifariki na wengijne kadhaa kujeruhiwa.

Watu sita wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho huku miito ikiongezeka ya kutaka mwanasiasa mmoja kutoka eneo hilo akamatwe kwa kuchochea vurugu hizo.

Taarifa ya Joseph Mwanjala 

Share This Article