Wakereketwa wa lugha ya Kiswahili nchini Kenya leo Jumanne wameungana na ulimwengu mzima kuadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) miaka mitano iliyopita liliitenga Julai 7 kila mwaka kuwa siku ya kuadhimishwa lugha hiyo duniani kote.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Kiswahili kwa ajili ya Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Kimataifa.”
Hapa nchini, siku hiyo inaadhimishwa katika Chuo Kikuu cha Kenyatta chini ya kaulimbiu “Kiswahili, Uwezo wa Wingilugha na Akili Unde katika Michezo na Uhifadhi wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu.”
Kwa upande mwingine, Shirika la Utangazaji nchini Kenya (KBC) kwa ushirikiano na shule ya upili ya Kenya High linaandaa maadhimisho mengine shuleni hapo.
Mada zinazozungumziwa ni pamoja na “Lugha ya Kiswahili na uwezeshaji wa vijana kwa uchumi na maarifa (Jinsi ubunifu wa kifasihi unavyoweza kuzalisha ajira na kuongeza thamani ya lugha ya Kiswahili”, na “Fasihi kama chombo cha amani na maridhiano (Jinsi riwaya, tamthlia ushairi na hadithi zinavyoelimisha utatuzi wa migogoro, uvumilivu na kuishi kwa amani).”
Lengo la maadhimisho hayo ni kuakisi umuhimu wa Kiswahili na hatua ambazo zimepigwa katika uenezi wa lugha hiyo katika sekta mbalimbali na nafasi yake katika jamii kwa sasa.
Hafla hiyo nayo inaandaliwa chini ya kaulimbiu “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Kiuchumi ya Kimataifa.”
Waandishi maarufu wa lugha ya Kiswahili kama vile Prof. Clara Momanyi na Dkt. Assumpta Matei ni miongoni mwa wanaohudhuria ambayo mgeni mheshimiwa ni msemaji wa serikali Isaac Mwaura.
Maadhimisho makubwa ya dunia yanafanyika katika makao makuu ya UNESCO jijini Paris nchini Ufaransa.
Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Aidha, Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi kote duniani kikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200.