Murkomen: Kenya na China zaimarisha ushirikiano wa kiusalama

Waziri huyo alichukua fursa hiyo kuihakikishia serikali ya China kwamba raia wa China wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya wako salama.

Tom Mathinji
2 Min Read
Kipchumba Murkomen - Waziri wa Usalama wa Taifa.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema Kenya na China zinaimarisha ushirikiano katika sekta ya usalama, kukabiliana na aina mpya za uhalifu kwa kutumia teknolojia.

Katika mkutano na Naibu Waziri wa Usalama wa Umma wa China Qi Yanjun ulioandaliwa  Jijini Lianyungang, Mkoa wa Jiangsu, Murkomen, alidokeza kuwa mataifa haya mawili yameshirikiana kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi na kuwaongezea uwezo wa kupambana na ugaidi pamoja na kukabiliana na uhalifu unaotekelezwa katika nchi mbalimbali.

Waziri huyo alichukua fursa hiyo kuihakikishia serikali ya China kwamba raia wa China wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya wako salama, wakiwa ni wanakandarasi na wafanyakazi wanaohusika katika miradi mbalimbali ya miundombinu hapa nchini.

“Nilihakikishia serikali ya China usalama wa raia wake wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya,” alisema Murkomen.

Waziri pia alisisitiza kuwa serikali imejitolea kulinda miradi muhimu, ikiwemo mradi wa  miundombinu unaounganisha Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini kupitia bandari ya Lamu (LAPSSET)  na ule wa kuboresha usafiri na biashara katika Upembe wa Afrika ambao unaendelea katika na maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Usalama wa China, alielezea imani yake katika juhudi za usalama  za Kenya, huku akiahidi kuendeleza ushirikiano na utoaji msaada kwa Huduma ya Taifa ya Polisi ya Kenya.

Katika mkutano huo, Murkomen alikuwa ameandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, na balozi wa Kenya nchini China Lynett Mwende miongoni mwa maafisa wengine.

Share This Article