Algeria imetangaza kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Muuungano wa Milki za Kiarabu (UAE), kwa kile imetaja kuwa misuru ya uchokozi na uhasama kutoka muungano huo.
Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria siku ya Alhamisi, vitendo hivyo vimefikia kiwango ambacho haviwezi tena kuvumiliwa, licha ya Algeria kutoa onyo mara kadhaa.
Wizara hiyo ilisema Algeria ilikuwa imefanya kila juhudi kulinda uhusiano wa nchi hizo mbili kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Balozi wa milki hizo alifika katika wizara hiyo na kuarifiwa rasmi kuhusu hatua hiyo, huku akipewa saa 48 kutekeleza uamuzi huo.
Huku ikijibu hatua hiyo ya Algeria, Anwar Gargash ambaye ni mshauri wa Rais wa UAE Mohammed bin Zayed, alisema uhusiano wa kidiplomasia unapswa kusuluhishwa kupitia mawasiliano na uwazi wa maslahi badala ya ishara ambazo zinahitaji kutafsiriwa.
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune, mara kadhaa ameishtumu UAE bila kuutaja moja kwa moja kwa kujaribu kuingilia maswala ya ndani na kudhoofisha uwezo wa mataifa katika kanda hiyo.