China yatoa wito wa ‘mazungumzo’ kusuluhisha mivutano ya biashara na Marekani

Martin Mwanje
2 Min Read
Marais Xi Jinping wa China na Donald Trump wa Marekani

China leo Alhamisi imetoa wito wa kufanywa kwa “mazungumzo” na Marekani ili kutatua mivutano inayoongezeka ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa duniani.

Tangu mapema mwaka huu, China na Marekani zimekuwa zikiwekeana ushuru wa forodha kwenye bidhaa zinazouzwa kati ya nchi hizo mbili.

“China daima imependekeza kuwa China na Marekani zinapaswa kukumbatia mtazamo chanya na ushirikiano kuelekea tofuati na utata katika nyanja za kiuchumi na kibiashara,” alisema msemaji wa Wizara ya Biashara He Yongqian wakati wa mkutano wa kila wiki na wanahabari.

“Lakini inapaswa kusisitizwa kuwa aina yoyote ya mawasiliano na mashauriano ni sharti yafanywe kwa kuzingatia heshima ya pande mbili, usawa na manufaa ya pande mbili,” alisema He.

“Matishio yanaweza kuwa tu bila tija. Natumai kuwa Marekani na China zitafanya kazi pamoja … kurejea kwenye njia sahihi ya kutatua masuala kupitia mazungumzo na mashauriano.”

Tangu alipoingia madarakani mwezi Januari mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump ameziwekea ushuru wa forodha nchi washirika wakuu wa biashara ikiwemo  China, Canada na Mexico.

Mwezi huu, Rais huyo wa Marekani aliongeza ushuru ambao awali aliwekea kwenye bidhaa za China kutoka asilimia 10 hadi 20.

China ilijibu kwa kuweka ushuru wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa mbalimbali za kilimo za Marekani ikiwa ni pamoja na maharage ya soya, nyama ya nguruwe na kuku.

China — ambayo ni mzalishaji kinara wa chuma duniani — pia iliapa jana Jumatano kuchukua “hatua zote stahiki” kulinda maslahi yake kufuatia ushuru mpya wa forodha uliowekwa na Marekani kwa chuma na alumini zinazoagizwa na nchi hiyo.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article