Chama cha DP kimetoa ilani ya siku 30 ya kuondoka kwenye muungano unaotawala wa Kenya Kwanza.
Chama hicho kinachohusishwa na Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ni miongoni mwa vyama tanzu vya muungano huo.
“Tafadhali zingatia kwamba kukaa kwetu katika muungano wa Kenya Kwanza hakuwezi kukastahimilika tena kutokana na hali ya kisiasa iliyopo kwa sasa,” alisema Katibu Mkuu wa chama cha DP Dkt. Jacob Haji kwenye barua aliyomwandikia Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Barua hiyo pia ilitiwa saini na mwenyekiti wa chama hicho Esau Kioni.
“Chama cha Democratic Party of Kenya kupitia barua hii, kinatoa ilani ya siku 30 ya kuondoka katika muungano huo kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha Kuondoka (8) katika makubaliano ya muungano,” iliongeza barua hiyo iliyoandikwa Machi 7 na kupokelewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa jana Jumatano.
Waziri Muturi ameibuka kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kenya Kwanza anayoituhumu kwa ongezeko la visa vya utekaji nyara wa watu wanaochukuliwa kuwa wakosoaji wa serikali hiyo.
Mwanawe Waziri huyo ni miongoni mwa waliotekwa nyara kabla ya kuachiliwa.