Hakikisho la Mbadi: Mipango inayofadhiliwa na Marekani haitakwama

Martin Mwanje
2 Min Read
John Mbadi - Waziri wa Fedha

Bajeti ya maendeleo itapunguzwa na fedha zitakazopatikana kutokana na upunguzaji huo kutumiwa kufadhili mipango itakayoathiriwa na usitishaji wa misaada ya kigeni uliotangazwa na Marekani siku chache zilizopita.

Hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Fedha John Mbadi.

Akiwahutubia wabahabari mjini Naivasha, Mbadi amesema ikiwa Rais Donald Trump atatekeleza tishio lake la kusitisha misaada ya kigeni kwa mipango mbalimbali ya maendeleo humu nchini, basi Kenya haitakuwa na budi bali kugeukia ufadhili wa ndani ya nchi.

“Hatutakuwa na budi ila kupunguza sehemu ya bajeti ya maendeleo na kutumia fedha hizo kufadhili mipango muhimu itkayoathiriwa na ukosefu wa fedha ikiwa misaada ya kigeni ya Marekani itasitishwa,” alidokeza Mbadi aliyezungumza baada ya kuhudhuria mkutano wa kati ya muhula wa Bunge la Taifa mjini Naivasha.

“Hakuna sababu ya kushtuka kwani nimeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha mipango ya afya ambayo ilitegemea mno misaada ya kigeni haitasambaratika.”

Aliongeza kuwa mipango ya afya kama vile ya Virusi vya Ukimwi ilikuwa muhimu katika kuokoa maisha na serikali itaifadhili kuhakikisha uendelevu wake.

Hata hivyo, Mbali aliongeza kuwa serikali bado inasubiri taarifa rasmi kutoka kwa Marekani juu ya usitishaji wa misaada hiyo ya kigeni.

“Rais Trump alichukua hatua punde alipoingia madarakani na ni kawaida kwa hilo kufanyika wakati serikali mpya inapoingia madarakani katika nchi yoyote,” alisema Waziri huyo.

Alikiri kuwa usitishaji wa misaada hiyo litakuwa pigo kubwa kwa Kenya.

Punde alipoingia madarakani mwezi jana, Trump alitia saini amri ya Rais ambayo ilisitisha mipango yote ya misaada ya kigeni inayotolewa na Marekani kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Lengo la hatua hiyo lilikuwa kubaini ikiwa misaada hiyo inawiana na malengo ya sera zake.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *