Ruto: Tunaondoa tamaduni kandamizi kwa elimu ya wasichana

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wakati wa uzinduzi wa shule katika eneo bunge la Langata, Nairobi

Serikali ya Kenya Kwanza inafanya kila iwezalo kuondoa tamaduni ambazo zimekuwa kikwazo kwa watoto wasichana kupata elimu nchini. 

Haya yamesema na Rais William Ruto wakati akiendelea na ziara yake ya wiki moja ya kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika kaunti ya Nairobi.

“Tunaondoa tamaduni zinazowazuia wasichana wetu kuhudhuria na kumaliza masomo,” alisema Rais Ruto leo Alhamisi asubuhi wakati akizindua shule ya upili ya wasichana ya PCEA Booth-Ngong’ Forest, kaunti ya Nairobi.

“Kupitia kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora, tunaweza tukaendeleza zaidi usawa wa jinsia na kuwawezesha wasichana wetu kushiriki ipasavyo katika kuibadilisha Kenya.”

 

 

Wakati wa uzinduzi wa shule hiyo, Rais Ruto aliahidi kufadhili masomo ya wasichana 10 kutoka familia zisizojiweza kutoka kila ya maeneo bunge 17 katika kaunti ya Nairobi kujiandikisha katika shule hiyo.

Ruto alikuwa ameandamana na Katibu katika Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na mbunge wa Langata Phelix Oduor almaarufu Jalang’o  miongoni mwa viongozi wengine.

 

 

Kiongozi wa nchi amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali na kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika kaunti ya Nairobi katika kipindi cha siku nne zilizopita.

Akizungumza katika eneo bunge la Dagoretti Kusini jana Jumatano, Ruto aliahidi kuwatumikia Wakenya wote kwa usawa wakati wa utawala wake.

Amewataka viongozi kutoka mirengo yote ya kisiasa kuyapa kipaumbele masuala ya maendeleo badala ya kujiingiza katika siasa za mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *