SHA yazindua mfumo wa kidijitali kuimarisha malipo ya huduma za afya

Waziri wa Afya Aden Duale, alisema mfumo huo utafanikisha uwazi na uwajibikaji.

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Afya Aden Duale azindua mpango wa kiditali wa Hakika, Jijini Nairobi.

Wizara ya Afya imezindua mfumo wa kidijitali wa utoaji kandarasi kati ya Halmashauri ya Afya ya Jamii SHA na vituo vya afya, ili kuimarisha ulipiaji wa huduma za Afya.

Akizindua mfumo huo kwa jina HAKIKA, katika hafla iliyoandaliwa kwenye Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC) Jijini Nairobi, Waziri wa Afya Aden Duale, alisema mfumo huo utafanikisha uwazi, uwajibikaji na utatatua wasiwasi wa wahudumu wa afya kuhusiana na kodi, utayarishaji wa taarifa za malipo na ucheleweshaji wa malipo.

Jukwaa hilo jipya la HAKIKA, pia litawezesha watoaji huduma za afya kutuma maombi yao, kupakua taarifa, kuthibitisha leseni zao, kutafuta kandarasi na kufuatilia harakati za kandarasi zao kupitia mtandaoni.

Aidha, Duale alisema Hakika itaonyesha huduma ambazo kila kituo cha afya kimeidhinishwa  kutoa na kupewa mkataba ili kuwasaidia wagonjwa kutambua vituo vilivyoidhinishwa kutoa huduma za afya.

Kupitia mfumo huo, wagonjwa watapata fursa ya kutoa maoni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwajibikaji na kuboresha huduma za afya.

Wakati huo huo, Duale alitoa wito wa kulipwa kwa haraka malipo yaliyoidhinishwa na kutoa sababu bayana kwa malipo yaliyokataliwa.

Mfumo huo wa HAKIKA, unaohudumu chini ya Halmashauri ya Afya ya Jamii SHA, utatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2029.

Share This Article