Kundi moja la kutoa misaada ya kibinadamu la Save the Children, limesema kuwa Sudan Kusini inakabiliwa na hatari ya ugonjwa wa kipindupindu, huku ghasia zikiendelea kughubika taifa hilo changa la bara Afrika.
Ugonjwa huo tayari umewaua watu 60 na kuwaambukiza takriban watu 2,600, tangu ulipozuka katika Jiji Kuu Juba mwezi Mei, ambapo majimbo 9 kati ya 10 yameripotiwa kunakili maambukizi ya ugonjwa huo.
Kulingana na kundi hilo, maambukizi ya kipindupindu huenda yakaongezeka huku mvua kubwa zikitarajiwa katika majuma kadhaa yajayo, likitoa wito wa juhudi za haraka kukabiliana na msambao huo.
Mkurugenzi wa kundi hilo Pete Walsh, alisema hali hiyo inahatarisha maisha ya raia wa taifa hilo, ikizingatiwa wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa chakula katika makazi ya muda yaliyo na msongamano.
Watoto wamo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu, lakini unaweza kutibiwa iwapo utagunduliwa mapema.