Uganda yatangaza haina ugonjwa wa Ebola

Tangazo hilo linajiri baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa siku 42, tangu mgonjwa wa mwisho wa Ebola aliporuhusiwa kwenda nyumbani Juni 16, 2026.

Tom Mathinji
2 Min Read
Chris Baryomunsi - Waziri wa Afya wa Uganda.

Waziri wa Afya wa Uganda Chris Baryomunsi, ametanga kuwa Uganda imefanikiwa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, na sasa taifa hilo la Afrika Mashariki halina maambukizi ya ugonjwa huo.

Kupitia kwa taarifa leo Jumanne, waziri huyo alisema, tangazo hilo linajiri baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa siku 42, tangu mgonjwa wa mwisho wa Ebola aliporuhusiwa kwenda nyumbani Juni 16, 2026.

“Kwenye kipindi hicho, Uganda ilitekeleza uchunguzi wa kitaifa dhidi ya ugonjwa huo na hakuna visa vipya vya Ebola ambavyo vimenakiliwa,” alisema Waziri huyo.

Kulingana na Baryomunsi, Uganda imefanikiwa kukabiliana na ugonjwa huo kutokana na jinsi serikali imewekeza kwenye mifumo ya afya, uwezo wa taifa hilo kutambua ugonjwa huo kwa haraka, ufuatiliaji wa waathiriwa, matibabu ya ubora wa hali ya juu na ushirikiano mwema na jamii.

Wakati huohuo alitoa tahadhari kwamba ugonjwa wa Ebola ungali hatari katika kanda hii, akidokeza kuwa Uganda inasalia kuwa makini katika sehemu za mpakani ikizingatiwa kuwa ugonjwa huo ungali unaenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Baryomunsi alisema Uganda na DRC zimetia saini Mkataba wa Makubaliano  wa kukabiliana na Ebola kwenye mipaka ya mataifa hayo, huku Uganda ikizindua maabara na kituo cha matibabu ya Ebola katika maeneo ya Aru na Kasenyi nchini DRC.

“Uganda sasa inawahakikishia raia wake, wageni, wawekezaji na Jamii ya Kimataifa kwamba ni salama, mifumo ya afya iko katika hali ya tahadhari na nchi hii iko wazi kwa utalii, biashara, na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi,” alidokeza Baryomunsi.

Uganda iliripoti kisa cha kwanza cha Ebola Mei 15,2026, mwathiriwa akiwa amesafiri kutoka DRC.

 

TAGGED:
Share This Article