Koome apewa tuzo ya Sejong ya mwanasheria bora

Jaji Mkuu amepokea tuzo hiyo kutokana na mchango wa majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi wa Mahakama ya Kenya.

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome, amepokea Tuzo ya kwanza ya Sejong ya Mwanasheria Bora kwa kutambua uongozi wake katika kuimarisha utawala wa sheria na kukuza upatikanaji wa haki unaomlenga mwananchi.

Tuzo hiyo imetolewa kwa pamoja na Mahakama ya Upeo ya Korea na Kundi la Benki ya Dunia, ikilenga utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na ushirikiano wa kimahakama.

Koome amekuwa wa kwanza kupokea tuzo hiyo kimataifa, hatua inayoiweka Kenya miongoni mwa nchi zilizotambuliwa wakati wa kuanzishwa kwa mpango huo wa kimataifa wa kutambua ubora katika sekta ya mahakama.

Tuzo hiyo imepatiwa jina la Mfalme Mkuu Sejong, mmoja wa viongozi wanaoheshimika zaidi nchini Korea na mwanzilishi wa Hangeul, mfumo wa uandishi wa Kikorea.

Urithi wake unahusishwa na kuhakikisha maarifa na taasisi za umma yanawafikia wananchi wa kawaida.

Kanuni hizo zimehusishwa na mpango wa Koome wa kustawisha mabadiliko kwa ajili ya upatikanaji wa haki yaani “Sustaining Transformation for Access to Justice, STAJ, unaolenga kuhakikisha haki inakuwa uzoefu halisi wa wananchi badala ya kubaki ahadi ya taasisi.

Chini ya uongozi wake, idara ya Mahakama ya Kenya imepanua huduma za haki kidijitali, usuluhishi, Mifumo Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro, Mahakama za Madai Madogo na mahakama maalumu zinazoshughulikia masuala ya watoto na jinsia.

Koome amepokea tuzo hiyo pia kwa kutambua mchango wa majaji, maafisa wa mahakama na wafanyakazi wa Mahakama ya Kenya.

Kituo cha usaidizi wa kisheria kwa mahusiano ya kifamilia cha Korea yaani “Korea Legal Aid Center for Family Relations” pia kimekuwa cha kwanza kupokea tuzo hiyo ya kwanza kitaifa, baada ya kutoa msaada wa kisheria na kulinda watu walio katika mazingira hatarishi kwa miaka 70.

Share This Article