Viongozi wa upinzani walipeleka saka saka zao za kura katika kaunti za Makueni, Kajiado na Taita Taveta walikofanya msururu wa mikutano ya kisiasa.
Ni wakati wa mikutano hiyo ambapo walimnyoshea kidole cha lawama Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Lorionokou.
Wakiongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, viongozi hao walielezea mashaka juu ya kushindwa kwa Lorionokou kuwapa Wakenya wanaotaka kusajili vyama vya kisiasa kadi za kusubiri kusajili vyama hivyo.
Kulingana nao, hii inaweza kudunisha haki ya kikatiba ya raia kushiriki katika siasa.
Wameahidi kutafuta majibu kutoka kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa wakiapa kutoruhusu mchakato huo kuingiliwa kati.
Matamshi yao yanakuja wakati ambapo kuna madai ya watu kadhaa kukimbilia kwenye ofisi hiyo na kuandikisha jina la vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Yamkini kivumbi cha kisheria huenda kikatifuka juu ya matumizi ya jina la Linda Mwananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Ikiwa mrengo wa Sifuna utapigwa marufuku kutumia jina hilo, basi itabidi utafute jina mbadala na kukabiliwa na kibarua cha kulinadi tena wakati ukipasha misuli ya kukabiliana na Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.