Rais William Ruto, amesema mechi za kuwania Taifa Bingwa Afrika (AFCON), zitakazoandaliwa nchini Kenya, zitakuwa za kusisimua na kuvutia.
Akizungumza Ijumaa jioni alipokutana na Rais wa CAF Patrice Motsepe katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa serikali inajizatiti kuhakikisha miundombinu itakayotumiwa kwa mechi hizo inakuwa tayari kwa wakati.
“Kwa upande wetu, tunahakikishia CAF kwamba tumejitolea kuwa mwenyeji wa mashindano ya kufana. Juhudi zimewekwa kuhakikisha miundombinu itakayotumiwa inakuwa tayari kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaohitajka,” alisema Rais Ruto.
Rai Ruto alisema Kenya itaonyesha mchezo wa soka wa hali ya juu kwa Afrika na dunia nzima, huku akielezea kuwa Wakenya watajitokeza kwa wingi kuonyesha mapenzi kwa mchezo wa soka wakati wa mashindano hayo.
Akiwa kwenye ziara ya kukagua utayari wa Kenya kwa mashindano ya AFCON ambayo Kenya itayaandaa kwa pamoja na Uganda na Tanzania mwezi Juni na Julai mwaka 2027, Rais wa CAF Patrice Motsepe, alipongeza Kenya kwa kutekeleza maandalizi ya kupigiwa mfano katika uwanja mpya wa michezo wa Talanta na ukarabati katika uwanja wa Kasarani.
Motsepe alidokeza kuwa CAF ina imani kwamba mataifa hayo ya Afrika Mashariki, yataandaa mashndano ya kufana.