KRA yanasa bidhaa za magendo za thamani ya shilingi milioni 46.77

Baadhi ya bidhaa zilizonaswa ni pamoja na sigara aina ya ORIS za thamani ya shilingi milioni 30.6,  Shisha ya thamani ya shilingi milioni 8.398, na maziwa ya unga ya thamani ya shilingi 7.768,

Tom Mathinji
1 Min Read
KRA yanasa bidhaa za magendo.

Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru hapa nchini  (KRA), imenasa bidhaa za magendo mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu, zinazoaminika zilikuwa zikiingizwa hapa nchini kutoka taifa moja jirani.

Kupitia kwa taarifa, KRA ilisema bidhaa hizo za thamani ya shilingi milioni 46.77, zilihatarisha taifa hili kupoteza ushuru wa hadi shilingi miliono 29.11.

KRA ilisema ilipokea habari za kijasusi kuhusu basi ambalo lilikuwa likisafirisha bidhaa hizo kupitia maeneo ya mpakani ambayo sio rasmi, ili zichukuliwe katika mpaka wa Busia na hatimaye zisafirishwe hadi Nairobi.

Maafisa wa KRA waliweka kizuizi cha barabarani kwa lengo la kunasa basi hilo, lakini dereva alihepa na kusababisha maafisa hao kulifuata na kulikamata katika eneo la Kondoo, Burnt Forest.

“Baadhi ya bidhaa zilizonaswa ni pamoja na sigara aina ya ORIS za thamani ya shilingi milioni 30.6,  Shisha ya thamani ya shilingi milioni 8.398, na maziwa ya unga ya thamani ya shilingi 7.768,” ilisema KRA kwenye taarifa.

KRA ilisema inaimarisha ukusanyaji habari kupitia ujasusi, ili kulinda afya ya umma, biashara halali dhidi ya ushindani haramu, kuimarisha mapato ya serikali na kushinikiza uzingatiaji wa sheria za ulipaji ushuru.

Share This Article