Kagwe akutana na Balozi wa UAE, wazungumzia kilimo na biashara

Martin Mwanje
1 Min Read
Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe akiwa na Balozi wa UAE humu nchini Dkt. Salim Ibrahim Alnaqbi

Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe leo Jumatatu amemtembelea Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) humu nchini Dkt. Salim Ibrahim Alnaqbi kwa lengo la kutafuta mbinu za kuimarisha ushirikiano wa kilimo na kibiashara kati ya nchi hizo mbili. 

Hususan, mazungumzo baina yao yaliangazia namna ya kuboresha uhusiano wa pande mbili na kutumia makubaliano yaliyofikiwa awali ili kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.

Mwezi Januari mwaka huu, Kenya na UAE zilitia saini Makubaliano ya Ushikiriano Mpana wa Kiuchumi (CEPA).

Makubaliano hayo yaliondoa vikwazo vya kibiashara na kufungua masoko mapya kwa ajili ya bidhaa za Kenya zinazouzwa nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na nyama, mbogamboga, matunda na maua.

Aidha, makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa kati ya Kenya na UAE mnamo mwaka 2023 yalipanua fursa za uwekezaji na hivyo kuiruhusu Kenya kusafirisha nchini humo bidhaa mbalimbali wakati ikiongeza idadi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka UAE kama vile bidhaa za eletroniki, mashine na magari.

Mkataba wa Maelewano kati ya Chama cha Taifa cha Wafanyabiashara nchini Kenya na Chama cha Kimataifa cha Dubai aidha unaunga mkono ushirikiano wa kibiashara kupitia shughuli za kibiashara na makongomano ya uwekezaji.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *