Serikali yaimarisha hatua za kukabiliana na Ebola

Hii ni kufuatia kuthibitishwa kwa kisa kimoja cha ugonjwa wa Ebola kilichomhusisha Mkenya aliyeishi nchini DRC kwa miaka 7 na kurejea nchini Jumamosi iliyopita.

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri wa Afya Aden Duale

Serikali ya Kenya imeimarisha hatua za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola nchini kote.

Hii ni baada ya kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kuthibitishwa nchini jana Jumanne.

Mwitikio wa kitaifa sasa unaangazia ufuatiliaji, uangalizi ulioboreshwa na kuboresha maandalizi katika mfumo wa afya.

Katika jumba la Afya leo Jumatano, Jopokazi la Kitaifa la Ugonjwa wa Virusi vya Ebola lilifanya mkutano wa kuratibu na kupitia upya hatua zinazohitajika za kukabiliana na ueneaji zaidi wa ugonjwa huo.

Jopokazi hilo limeongeza jitihada za ufuatiliaji na uangalizi katika maeneo ya kuingia nchini na utayari wa vituo vya afya vilivyotengwa ili kuwafuatilia wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa wa Ebola.

Mwitiko huo unafanywa kwa ushirikiano na serikali za kaunti, washirika wa maendeleo na washirika wengine wa kiufundi na kibinadamu.

Akiongoza mkutano huo, Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alitoa wito kwa Wakenya kusalia watulivu na waangalifu na kufuatilia taarifa zinazotolewa kupitia njia rasmi za Wizara ya Afya wakati mwitikio wa kitaifa ukiimarishwa.

Baadaye, Waziri wa Afya Aden Duale aliwaongoza maafisa wa wizara hiyo katika kukagua kituo kilichotengwa cha kuwatibu wagonjwa wa Ebola katika Nairobi Hospital.

Ukaguzi huo ni sehemu ya hatua zinazoendelea za kuimarisha maandalizi na mwitikio wa nchi katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Kituo hicho chenye vitanda 133 ni miongoni mwa vituo vilivyotengwa kusaidia katika kutenga na kutibu watu wanaoshukiwa na waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya korona.

 

Share This Article