Msimu wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka 2024/2025, utakamilika leo Juni 22, kwa mechi za mzunguko wa 34.
Police FC ambao wametwaa ubingwa wa Ligi hiyo kwa mara kwanza watafunga msimu dhidi ya mabingwa wanaoondoka Gor Mahia katika uwanja wa Ulinzi .
Hata hivyo, Kinyang’anyiro kitakuwa katika nafasi za kushushwa ngazi Bidco United, Murang’a Seal, Nairobi City Stars, Posta Rangers na Talanta FC.
Bidco United wanaoburura mkia watakuwa uwanjani Dandora dhidi ya Sofapaka, kuanzia saa tisa wakihitaji ushindi ili kuwa na nafasi ya kujisalimisha.
Murang’a Seal walio katika nafasi ya pili kutoka mwisho hawana budi kuwashinda Talanta FC, katika uwanja wa Sportpesa ili kuwa na uwezo wa kusalia ligini msimu ujao.
Nairobi City Stars watakuwa uwanja wa manispaa wa Thika dhidi ya Mathare United.
Talanta FC ni ya 14 kwa alama 35, pointi moja zaidi ya Posta, City Stars na Murang’a huku Bidco wakishika mkia kwa alama 32.
Tusker FC, Kakamega Homeboyz na Gor Mahia watawania nafasi ya pili, Gor wakikabiliana na mabingwa wateule Police FC katika uwanja wa Ulinzi, nayo Homeboyz ikiwe nyumbani Mumias dhidi ya Tusker FC.
Polisi walitwaa ubingwa kwa mara ya kwanza wiki jana, wanaongoza jedwali kwa pointi 64, wakifuatwa na Gor kwa alama 58.
Homeboyz ni tatu kwa alama 57, alama moja zaidi ya Tusker FC iliyo ya nne.