Seneti yatilia shaka pengo la ufadhili uwanja wa Nyayo

Kandarasi ya ukarabati wa uwanja huo ni ya thamani ya Shilingi Bilioni 1.184, lakini ni Shilingi milioni 200 pekee zimelipwa.

Marion Bosire
2 Min Read
Julius Murgor, Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Leba na Ustawi wa Jamii

Kamati ya Seneti kuhusu Leba na Ustawi wa Jamii imeelezea wasiwasi kuhusu upungufu wa Shilingi milioni 984 katika ukarabati wa Uwanja wa michezo wa Nyayo, jijini Nairobi.

Kamati ilifahamishwa kwamba mkandarasi kwa sasa hayupo katika eneo la ujenzi baada ya kazi kusimamishwa kusubiri malipo.

Mkataba huo una thamani ya Shilingi Bilioni 1.184, ambapo ni Shilingi milioni 200 pekee ambazo zimelipwa hadi sasa.

Uwanja wa Nyayo unatarajiwa kutumika kama eneo la mazoezi wakati wa michuano ya AFCON 2027. Kazi za mifereji ya maji, taa za uwanjani na uboreshaji wa kamera za CCTV zimekamilika.

Kazi ambazo bado hazijakamilika ni pamoja na kuunganisha taa kwenye gridi ya taifa, kufunga skrini za LED na ubao wa matokeo, kukamilisha uzio wa uwanja, milango ya kuingilia na mifumo ya tiketi na kuboresha miundombinu kwa watu wenye ulemavu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seneta Julius Murgor wa West Pokot, alitoa wito wa ushirikiano wa karibu kati ya wizara, idara na mashirika ya serikali yanayohusika na maandalizi hayo, hasa kuhusu ufikivu, usalama kazini na maandalizi ya dharura.

Kamati hiyo itajumuisha matokeo ya ukaguzi wa Uwanja wa Nyayo na ziara yake ya hivi karibuni katika Uwanja wa Talanta katika ripoti itakayoongoza majadiliano na wizara husika pamoja na Hazina ya Taifa kuhusu ufadhili unaohitajika kabla ya AFCON 2027.

Share This Article