Mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva nchini Tanzania, Hamisi Ramadhan, maarufu kama H Baba, amempongeza binti yake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo amempongeza binti yake kwa jina Tanzanite baada ya kuhitimu elimu ya Darasa la Saba.
Katika ujumbe wake, H Baba amempongeza binti yake na kumwombea ulinzi na mwongozo wa Mwenyezi Mungu katika hatua inayofuata ya masomo yake.
“Hongera binti yangu kwa kuhitimu Darasa la Saba. Allah akulinde, Allah akuongoze vyema. Kikubwa ushajua baba yako ni mtu wa aina gani, hapendi nini na nini,” ameandika H Baba.
Msanii huyo pia ameeleza kuwa amekuwa akipambana kwa ajili ya watoto wake, Tanzanite na mdogo wake Africa, tangu walipozaliwa, huku akimtakia binti yake mafanikio zaidi katika masomo.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, H Baba ameandika: “Maji yakishamwagika hayazoleki,” akirejelea nasaha ambazo amekuwa akiwapa watoto wake kuhusu maisha na maamuzi yao.