Bien kutumbuiza katika tamasha ya Afro Fest nchini Marekani

Itaandaliwa Septemba 4 hadi 6, 2026 katika uwanja wa matamasha wa Northwest Stadium, jijini Washington D.C, Marekani.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii nyota wa muziki wa Kenya, Bien-Aimé Baraza, maarufu kama Bien, anatarajiwa kuendelea kupeperusha bendera ya muziki wa Afrika Mashariki kimataifa.

Hii ni baada yake kutangazwa kuwa mmoja wa wasanii watakaotumbuiza katika tamasha ijayo ya Afro+ Fest 2026 nchini Marekani.

Mwanachama huyo wa zamani wa kundi la Sauti Sol atatumbuiza na baadhi ya wanamumuziki wengine wa Afrika, akiwemo Davido, Wizkid, Tems, Tiwa Savage na Ayra Starr.

Tamasha hiyo itakuwa ya siku tatu kuanzia Septemba 4 hadi 6 katika uwanja wa matamasha wa Northwest Stadium, jijini Washington D.C.

Tangazo hilo linaongeza mafanikio makubwa katika safari ya Bien kama msanii wa kujitegemea, iliyomletea utambuzi duniani kupitia nyimbo zake zilizofanya vizuri, ushirikiano na wasanii wa kimataifa na maonyesho yaliyovutia maelfu ya mashabiki barani Afrika, Ulaya na Amerika Kaskazini.

Hii ni fursa nyingine kwa msanii huyo wa Kenya kutangaza muziki wa Afrika Mashariki kwenye moja ya majukwaa makubwa zaidi ya Waafrika wanaoishi ughaibuni.

Tamasha hiyo huadhimisha utamaduni wa Afrika na Karibiani kupitia muziki, mitindo, vyakula na sanaa, huku ikivutia mashabiki wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani kila mwaka.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Bien kutumbuiza katika tamasha ya Afro Nation ya Portugal mwaka 2026, ambako aliiwakilisha Kenya pamoja na wasanii wengine wakubwa kutoka Afrika, akiendelea kujiimarisha kama mmoja wa wanamuziki wa Afrika wanaozidi kupata umaarufu kimataifa.

Share This Article