Maadhimisho ya miaka 20 ya King James

Anaandaa tamasha kubwa itakayofanyika Jumamosi, Agosti 1, 2026, katika ukumbi wa BK Arena jijini Kigali.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii maarufu wa R&B na Afrobeat mzaliwa wa Rwanda, King James, atasherehekea miaka 20 ya safari yake ya muziki kupitia tamasha kubwa itakayofanyika Jumamosi, Agosti 1, 2026, katika ukumbi wa BK Arena jijini Kigali.

Msanii huyo ametangaza kuwa tamasha hiyo itakuwa heshima kwa mafanikio yake ya muda mrefu yaliyojengwa kupitia nyimbo zilizofanya vizuri, maonyesho yenye nguvu jukwaani na uhusiano wa kudumu na mashabiki wake.

Waandaaji wanatarajia maelfu ya wapenzi wa muziki kuhudhuria hafla hiyo, wakieleza kuwa ni moja ya matukio makubwa zaidi ya burudani mwaka huu nchini humo.

Maandalizi tayari yanaendelea, mafundi wa mitambo wakikiahidi mfumo wa sauti wa kiwango cha kimataifa, mwangaza wa kisasa na jukwaa la kuvutia.

Hadi sasa, majina ya wasanii wageni yatakaoshiriki hayajatangazwa rasmi, ingawa hamasa inaendelea kuongezeka nchini Rwanda na mataifa jirani.

Tamasha hiyo itaadhimisha ukuaji wake wa kisanii na kuonyesha mchango wake mkubwa katika maendeleo ya muziki wa kisasa wa Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa tasnia ya muziki wanaamini kuwa maonyesho hayo yatakuwa hatua nyingine muhimu katika historia ya King James, yakizidi kuimarisha sifa yake kama mmoja wa wasanii wanaoheshimika zaidi katika ukanda huu.

Mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki wanatarajiwa kusafiri kwenda Kigali kushuhudia tamasha hiyo ya kihistoria na kusherehekea msanii ambaye ubunifu na uthabiti wake vimeacha alama kwa miaka ishirini.

Share This Article