KBC Radio Taifa yaacha alama kwa jamii Kakamega

Ziara ya siku mbili ilijumuisha elimu, burudani na huduma kwa jamii.

Francis Ngala
6 Min Read
Watangazaji wa KBC Radio Taifa wakiwa Jukwaani, Shule ya wasichana ya Butere; Picha - Selestus Mayira.

Kwa siku mbili mfululizo, Kaunti ya Kakamega ilikuwa kitovu cha elimu, burudani na huduma kwa jamii huku KBC Radio Taifa ikiwaleta pamoja viongozi, wanafunzi na wasikilizaji kupitia shughuli mbalimbali zilizoimarisha uhusiano kati ya kituo hicho na jamii.

Ziara hiyo iliyoongozwa na Msimamizi wa Kituo cha Radio Taifa Rebecca Cherotich, iliwaleta pamoja watangazaji wa kituo hicho, wasikilizaji, viongozi wa serikali pamoja na wanafunzi katika shughuli mbalimbali zilizolenga kuimarisha uhusiano kati ya KBC Radio Taifa na jamii.

Shughuli zilianza Ijumaa asubuhi 24,2026 kwa matangazo ya moja kwa moja ya kipindi cha Zinga yaliyofanyika  Khetias Poa Supermarket mjini Kakamega.

Mtangazaji wa KBC Dorah Manya akimhoji Gavana Fernandes Barasa, Kakamega ; Picha – Selestus Mayira

Wasikilizaji walijitokeza kwa wingi kushiriki katika kipindi hicho, kukutana na watangazaji wao na kujishindia vikapu vya zawadi, muda wa maongezi pamoja na zawadi nyingine mbalimbali.

Kipindi hicho kilichoendeshwa na Dorah Manya, kilimualika Gavana wa Kaunti ya Kakamega, Fernandes Barasa kwa mahojiano ya Kipekee, ambaye aliipongeza KBC Radio Taifa kwa kuendelea kurusha vipindi vyenye uwiano, vinavyoelimisha na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

Katika mahojiano hayo, gavana huyo alieleza mafanikio yaliyofikiwa na serikali yake pamoja na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Kakamega na Serikali ya Kitaifa katika kuharakisha maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Jukumu langu kubwa ni kuunganisha wana Kakamega wote,Vile Rais Ruto amejaribu kuunganisha Taifa zima pia mimi ni kujaribu kuunganisha viongozi wote wa Kakamega. Ni vyema Kushirikiana na nashirikiana na serikali kuu kwa masuala ya maendeleo” alisema Gavana Barasa.

Gavana Wa Kakamega Fernandes Barasa ; Picha – Selestus Mayira. 

Katika kuendeleza wajibu wake kwa jamii, KBC Radio Taifa kwa ushirikiano na Wizara ya Utumishi wa Umma ilitoa msaada wa taulo za usafi kwa wasichana, unga wa uji, sabuni, blanketi pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa wanafunzi wa Malava Special Unit na Emusala Special Unit.

KBC Radio Taifa ikiwasilisha Bidhaa muhimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum shule ya Malava Special Unit; Picha-Selestus Mayira.

Msaada huo uliwaletea faraja na tabasamu wanafunzi wenye mahitaji maalum, huku ukidhihirisha azma ya KBC Radio Taifa ya kuendelea kushirikiana na jamii na kuwafikia walio katika mazingira yanayohitaji msaada.

KBC Radio Taifa ikiwasilisha Bidhaa muhimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum shule ya Emusala Comprehensive Special Unit; Picha-Selestus Mayira.

Baadaye jioni, shughuli za Siku ya Ijumaa 24, 2026 zilihitimishwa kwa Usiku wa Rhumba uliofanyika Havannas Lounge, ambapo watangazaji wa KBC wakiongozwa na Mfumu Kimbangu maarufu kama Mzairwa, Isaac Lemoka, DJ Stano, Mathias Momanyi na Caroline Mramba, walishirikiana kuwaburudisha wapenzi wa Muziki wa Rhumba.

Wapenzi wa Muziki wa Rhumba wakiburudika Havannas lounge, Kakamega; Picha – Selestus Mayira.

Siku ya Jumamosi, shughuli zilihamia Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere ambako kipindi cha Ramani ya Kiswahili kilirushwa mubashara.

Kipindi hicho kilichoongozwa na Mathias Momanyi akisaidiwa na Dorah Manya na Isaac Lemoka, kilitoa jukwaa la kuhamasisha matumizi ya Kiswahili sanifu kupitia mijadala, maswali na majibu pamoja na shughuli mbalimbali za kielimu.

Wanafunzi wa Butere Girls; Picha – Selestus Mayira.

Mbali na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere kipindi hicho pia kiliwashirikisha wanafunzi kutoka Shule ya Upili ya Wavulana ya Butere, Shule ya Upili ya Wasichana ya Buchenya na Shule ya Upili ya Wavulana ya Mabole, hatua iliyochangia kubadilishana maarifa na kuendeleza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya umoja wa kitaifa.

Meneja wa Chapa (KBC Brand Manager) Jackline Aseka; Picha -Selestus Mayira.

Akihitimisha shughuli hiyo, Meneja wa Chapa wa KBC (KBC Brand Manager) Jackline Aseka, aliupongeza uongozi wa Shule ya Upili ya wasichana ya Butere kwa kuwapokea watangazaji wa KBC Radio Taifa na kwa kuwaalika wanafunzi kutoka shule jirani kushiriki katika kipindi hicho.

Alisema hatua hiyo imeongeza wigo wa ujifunzaji na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanafunzi.

Aidha, aliwahimiza wanafunzi kuzingatia masomo na kudumisha nidhamu ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Wanafunzi, tieni bidii katika masomo yenu na muwe watiifu kwa walimu ili kufikia malengo yenu,” alisema Aseka

Ziara hiyo ya siku mbili ilidhihirisha nafasi ya KBC Radio Taifa kama chombo cha utangazaji kinachounganisha wananchi kupitia habari, elimu na burudani, huku kikitekeleza wajibu wake kwa jamii.

Kupitia mahojiano na viongozi, msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, burudani ya Muziki wa Rhumba na kuhamasisha matumizi ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, ziara ya Kakamega iliimarisha zaidi uhusiano kati ya KBC Radio Taifa na wasikilizaji wake.

Kwa mara nyingine, KBC Radio Taifa imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama Sauti ya Mkenya redio inayohabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kushirikiana na jamii katika kujenga taifa.

Share This Article
Follow:
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.